TheHItDotCom

TheHItDotCom
we bring you news to your hand

Monday, May 27, 2013

Waliofeli kidato cha nne meno nje, ufaulu sasa waongezeka

 

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako

Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.

Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.


MATOKEO KIDATO CHA SITA: SIFURI KIBAO ZAFUTWA KIMYAKIMYA

MPANGILIO wa alama mpya za kufaulu kwa wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka jana, ambao matokeo ya mitihani yao yanaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, unadaiwa kuzua aibu na kama si uamuzi uliotajwa bungeni wa matumizi ya alama za ufaulu za zamani, matokeo hayo yangeibua aibu kama ilivyojitokeza kwa kidato cha nne, 2012.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambalo linaendelea kupanga matokeo hayo ya kidato cha sita kwa kuzingatia alama za zamani kama ambavyo taarifa ya awali ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilivyosomwa bungeni hivi karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi katika ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia uhai wa vyuo vikuu nchini kukosa wanafunzi wa kutosha.

“Hali ilikuwa mbaya sana kama alama za kufaulu zingeachwa zitumike zile mpya na si za zamani. Vyuo vikuu nchini visingeweza kupata wanafunzi wa kutosha. Tatizo hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu mitihani bali ni kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa. Alama hizi zilipaswa kuanza kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza kidato cha kwanza wawe wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama mpya na waendelee nazo hadi mitihano yao ya mwisho.

“Na hivyo hivyo kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Alama hizi mpya zinapaswa kutumika kwako kuanzia wakiwa kidato cha tano mara wanapoanza shule, kila mitihani wanayopewa isahihishwe na kupangiwa alama kwa kutumia hizi alama mpya,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka NECTA.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika awali ni daraja F kuanzia 34 hadi sifuri; badala ya alama hiyo F kuanzia 20 hadi 0; daraja D kwa kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia 35 tofauti na awali, yaani alama 21.

Taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, kati ya sababu za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita tofauti na muda uliotarajiwa yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na upangaji upya matokeo hayo, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato cha nne ambapo matokeo yalitangazwa na kisha kufutwa ili kuyapanga upya kwa kutumia alama za zamani.

Lakini alipoulizwa kuhusu masuala hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa Taasisi hiyo nyeti nchini, John Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu kwamba mchakato wa kuandaa matokeo ya kidato cha sita unaendelea, siwezi kusema lini hasa utakamilika lakini nina uhakika ni katika muda muafaka.”

Kuhusu matokeo ya kidato cha sita kucheleweshwa kutokana kupangwa upya ili kupunguza idadi ya waliofeli kutokana na matumizi ya alama mpya za kufaulu, Nchimbi anasema; “Unajua haya maagizo haya ya bungeni (kupanga matokeo kwa kuzingatia alama za zamani) yamekuja wakati mchakato wa kuandaa matokeo ulikwishaanza. Kwa hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya kazi hiyo tena kwa kufuata maagizo hayo.”

Hata hivyo, hakuweka bayana kama matokeo ya awali kabla ya maagizo ya Serikali yaliyotolewa bungeni kutumia alama za zamani yamewafanya wanafunzi wengi kufeli na badala yake akasema; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo hayo haukuwa umefika mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa hiyo si sahihi kusema rasmi walifeli.”

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa matokeo yanayotarajiwa ya kidato cha sita, taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, baada agizo la serikali la kufuta na kurejewa upya kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, takriban wanafunzi 50,000 wamepata unafuu katika matokeo yao tofauti na awali.