TheHItDotCom

TheHItDotCom
we bring you news to your hand

Thursday, May 30, 2013

Wanafunzi Mzumbe Sekondari waandamana usiku wa manane


Wanafunzi zaidi ya 600 wa Shule ya Sekondari Wavulana ya Vipaji Maalum ya Mzumbe, iliyopo wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, jana walitembea zaidi ya kilometa 20 kwa maandamano kwenda kwa Mkuu wa Mkoa huo kwa lengo la kumfikishia kero zao.

Miongoni mwa kero hizo ni ubovu wa miundombinu na lugha chafu zinazodaiwa kutolewa na baadhi ya walimu wa shule hiyo.

Maandamano ya wanafunzi hao yalianzia shuleni hapo majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia jana.

Hata hivyo, yalizuiwa na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) pamoja na wa Kikosi cha Usalama Barabarani kabla ya kufika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa.

Askari hao waliingilia kati maandamano hayo baada ya kufika katika kijiji cha Kasanga Maliasili, ambako wanafunzi hao walifunga barabara kuu ya Morogoro-Iringa upande mmoja kwa zaidi ya saa 10.

Askari hao waliwaomba wanafunzi hao kukaa upande mmoja wa barabara ili kuruhusu magari kuendelea na safari zake.

Wanafunzi hao wakiwa wamezuiwa na askari hao, Katibu Tawala wa Mkoa, Elia Ntandu, alifika katika kijiji hicho kwa nia ya kuzungumza nao.

Hata hivyo, wanafunzi hao walikataa kuzungumza naye, badala yake waliendelea kung’ang’ania kutaka waachiwe kwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, ambaye yuko nje ya mkoa kikazi.

Hali hiyo ilisababisha kuzuka mvutano mkubwa uliodumu kwa zaidi ya saa mbili kabla mwafaka kufikiwa.

Mwafaka huo ulikwenda sambamba na wanafunzi hao kukubali kuzungumza na Katibu Tawala huyo, ambao walitumia nafasi hiyo kumueleza kero zote zinazowakabili.
Walimuomba azitafutie ufumbuzi kero hizo, ikiwa ni pamoja na kutaka Mkuu wa Shule hiyo, Dismas Njawa, pamoja na kabineti yake yote, wahamishwe.
 Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wanafunzi Emil Mayani na Paschal Francisco, walimwambia Katibu Tawala huyo kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo miundombinu mibovu na choo.

Walisema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 600 ina matundu matano tu ya vyoo na kwamba kila tundu hutumiwa na wastani wa wanafunzi 150, hali ambayo walidai ina hatarisha usalama wa afya zao kutokana na matundu hayo machache kujaa na kuwa kwenye mazingira yasiyoridhisha.
Pia walidai mabafu wanayotumia hayana milango na hivyo kulazimika kuziba na taulo mlangoni wanapooga.

Aidha, walidai mabweni wanayotumia ni machakavu na baadhi yake hayana umeme. Walidai hali hiyo imekuwa ikiwafanya wasome katika mazingira magumu.

Walitaja kero nyingine kuwa ni chakula kibaya kisichofaa kuliwa na binadamu na ubadhilifu wa fedha za shule.

Walisema shule hiyo ina vyanzo vingi vya mapato, lakini kila wanapohoji matumizi yake, uongozi wa shule umekuwa ukiwapa majibu yasiyoridhisha.

Kwa mujibu wa wanafunzi hao, vyanzo vya mapato vilivyopo vinatosha kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibika shuleni hapo.

Baadhi ya vyanzo hivyo walivitaja kuwa ni soko, maduka yanayolizunguka soko hilo, uwanja wa mpira pamoja na ukumbi wa shule hiyo.

Walidai ukumbi huo umekuwa ukikodishwa kwa ajili ya shughuli mbalimbli, ikiwamo sherehe.

Kero nyingine ni ukosefu wa mwalimu wa somo la Fizikia kwa kidato cha tano na kwamba tangu wameanza masomo ya kidato hicho hawajawahi kulisoma.

Kutokana na hali hiyo, walihoji ikiwa hakuna mwalimu wa kuwafundisha kwanini wasikodi mwingine kwa kuwa wanalipa Sh. 10,000, ambazo ni fedha za taaluma.

Waliwalalamikia baadhi ya walimu kwa kukosa kuwajibika ipasavyo na wengine kuwapa muhtasari wa masomo na kusahihisha na kudai kuwa ndiyo mazoezi yenyewe, hivyo kuhoji kama hizo ndizo taratibu za ufundishaji.

Lugha chafu walizodai kutolewa na mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, walizitaja kwa Katibu Tawala huyo, lakini kutokana na maadili ya Kitanzania haziwezi kuandikwa gazetini.

Walisema wamekuwa wakitoa malalamiko mara kwa mara kwenye uongozi wa shule, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, hali hiyo imesababisha uwakilishi wa wanafunzi, ambao ni viongozi kuamua kujiuzulu nyadhifa zao.

Walimuomba Katibu Tawala huyo kumhamisha mkuu wa shule, msaidizi wake, mwalimu wa malezi, taaluma na nidhamu.

Mkuu wa Shule hiyo, Njawa, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alisema kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha wao siyo wakaguzi wa shule, hivyo walichoeleza wanafunzi hao siyo sahihi.

Alisema mambo mengine yaliyodaiwa na wanafunzi hao, ikiwamo chakula, hayana ukweli na kwamba, kila kitu kiko kwenye hali nzuri na kwamba yote yaliyodaiwa wanafunzi ni uzushi wa wanafunzi wachache.

“Hatuna vitu kama hivyo. Huo ni uwongo tu. Hao watoto msiwaendekeze. Wataharibu vitu. Mimi siwezi kuwanyanyasa,” alisema na kuongeza:

“Hawawezi kukaa kwenye mazingira mabaya. Mwalimu wa Fizikia yupo, isipokuwa alikuwa na masuala binafsi. Siyo kwamba, hawana.”

No comments:

Post a Comment