MPANGILIO wa alama mpya za kufaulu kwa wahitimu wa kidato cha sita
waliohitimu mwaka jana, ambao matokeo ya mitihani yao yanaweza
kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, unadaiwa kuzua aibu na kama si
uamuzi uliotajwa bungeni wa matumizi ya alama za ufaulu za zamani,
matokeo hayo yangeibua aibu kama ilivyojitokeza kwa kidato cha nne,
2012.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka Baraza la Taifa la Mitihani
(NECTA) ambalo linaendelea kupanga matokeo hayo ya kidato cha sita kwa
kuzingatia alama za zamani kama ambavyo taarifa ya awali ya Tume
iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilivyosomwa bungeni hivi
karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi katika ufaulu kwa wanafunzi wa
kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia uhai wa vyuo vikuu nchini
kukosa wanafunzi wa kutosha.
“Hali ilikuwa mbaya sana kama alama za kufaulu zingeachwa zitumike zile
mpya na si za zamani. Vyuo vikuu nchini visingeweza kupata wanafunzi wa
kutosha. Tatizo hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu
mitihani bali ni kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa. Alama
hizi zilipaswa kuanza kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza
kidato cha kwanza wawe wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama
mpya na waendelee nazo hadi mitihano yao ya mwisho.
“Na hivyo hivyo kwa wanafunzi wa kidato cha sita. Alama hizi mpya
zinapaswa kutumika kwako kuanzia wakiwa kidato cha tano mara wanapoanza
shule, kila mitihani wanayopewa isahihishwe na kupangiwa alama kwa
kutumia hizi alama mpya,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka
NECTA.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika
awali ni daraja F kuanzia 34 hadi sifuri; badala ya alama hiyo F
kuanzia 20 hadi 0; daraja D kwa kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia
35 tofauti na awali, yaani alama 21.
Taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, kati ya sababu za kuchelewa
kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita tofauti na muda uliotarajiwa
yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na upangaji upya matokeo hayo, ikiwa
ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato cha nne ambapo matokeo yalitangazwa
na kisha kufutwa ili kuyapanga upya kwa kutumia alama za zamani.
Lakini alipoulizwa kuhusu masuala hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa
Taasisi hiyo nyeti nchini, John Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu
kwamba mchakato wa kuandaa matokeo ya kidato cha sita unaendelea, siwezi
kusema lini hasa utakamilika lakini nina uhakika ni katika muda
muafaka.”
Kuhusu matokeo ya kidato cha sita kucheleweshwa kutokana kupangwa upya
ili kupunguza idadi ya waliofeli kutokana na matumizi ya alama mpya za
kufaulu, Nchimbi anasema; “Unajua haya maagizo haya ya bungeni (kupanga
matokeo kwa kuzingatia alama za zamani) yamekuja wakati mchakato wa
kuandaa matokeo ulikwishaanza. Kwa hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya
kazi hiyo tena kwa kufuata maagizo hayo.”
Hata hivyo, hakuweka bayana kama matokeo ya awali kabla ya maagizo ya
Serikali yaliyotolewa bungeni kutumia alama za zamani yamewafanya
wanafunzi wengi kufeli na badala yake akasema; “Hilo siwezi
kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo hayo haukuwa umefika
mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa hiyo si sahihi kusema
rasmi walifeli.”
Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa matokeo yanayotarajiwa ya
kidato cha sita, taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa, baada agizo la
serikali la kufuta na kurejewa upya kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka
2012, takriban wanafunzi 50,000 wamepata unafuu katika matokeo yao
tofauti na awali.
No comments:
Post a Comment