TheHItDotCom

TheHItDotCom
we bring you news to your hand

Wednesday, May 29, 2013

WARAKA WA SHULE YA SEKONDARI MZUMBE KWA MKUU WA MKOA WA MOROGORO

-->
UTANGULIZI
Shule ya sekondari Mzumbe  ni moja kati ya shule maalumu nchini Tanzania. Ni shule ambayo inasfika kote Tanzania kwa taaluma na nidhamu yake safi. Kwa kuthibitisha hayo, viongozi wengi bora wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni matunda ya shule hii.
Kwa sifa hiyo,sisi wanafunzi wa shule ya sekondari Mzumbe tunajivunia kuwepo shuleni hapa na tunajitahidi kutimiza wajibu wetu ili kutunza na kuendeleza sifa ya shule hii kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla. Tukiwa na wajibu huo mzito, tunahitaji mazingira bora ya kujifunzia kama vile vifaa na nyenzo bora za kitaaluma, uongozi bora na ushirikiano chanya baina ya wanafunzi na walimu.
Hata hivyo, hali ya maisha ya hapa shuleni kwa sasa inazidi kuwa mbaya kiasi cha kuwa kipingamizi katika juhudi za kutimiza malengo yetu, katika kutimiza malengo yetu ya kulijenga taifa kama yalivyo matumaini ya watanzania wote.
Pamoja na hali hiyo tumejitahidi kukabiliana na matatizo mengi yaliyopo kwa njia mbalimbali hususani kufanya mazungumzo na kushauriana na uongozi wa shule kwa kuzingatia itifaki bila ya mafanikio yoyote.
Kutokana hali hiyo, sisi wanafunzi wa shule ya sekondari Mzumbe tumefikia uamuzi wa kuandika waraka unaoeleza matatizo yanayotukabili ambayo tumeyabainisha katika vipengele vifuatavyo:
1.      Mapato na matumizi ya shule
Kama wanafunzi tuna haki ya kushirikishwa katika taarifa za mapato na matumizi ya shule yetu. Shule ina vyanzo mbalimbali vya mapato kama vile ukumbi wa shule unaokodishwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali, ushuru kutoka katika magenge na maduka (soko la Mzumbe sekondari), mashamba yanayokodishwa, ada ya kituo kwa wanafunzi wanaorudia mitihani pamoja  na kituo cha masomo ya jioni kilichopo ndani ya eneo la shule (Mzumbe evening class). Pamoja na hayo,  hatupewi taarifa juu ya pesa zinazotokana na miradi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, tumebaini kuwa kutotolewa kwa taarifa ya mapato na matumizi kumesababisha ubadhilifu na ufisadi  unaoendelea hapa shuleni.
2.      Afya
Ni wazi kuwa, afya bora ni muhimu kawa mwanadamu yoyote ili aweze kutimiza wajibu wake. Lakini kwa sasa suala la afya limekuwa tatizo kubwa hapa shuleni. Mfano: utaratibu mbovu wa matibabbu, ambapo kuna mlolongo mrefu sana katika ufuatiliaji wa huduma za matibabu, ikiwemo kutotolewa kwa fedha za matibabu haliinayotulazimu kutumia fedha zetu za mifukoni ambazo hatahivyo huwa hatulipwi, licha ya kuwa tulikwisha lipia awali f edha za matibabu.
Kukosekana kwa dawa hata zile za muhimu katika zahanati ya shule limekuwa tatizo sugu.Hivyo, tumekuwa tukilazimika kununua dawa katika maduka ya madawa.
Kutokana na ubovu na uchakavu wa zahanati yetu, hali ya zahanati hiyo ni ya kusikitisha sana, kwani  inashindikana hata kutoa huduma ndogo ndogo za kiafya.
Pia, hali mbaya ya vyoo na mabafu yetu ni tishio kwa afya zetu. Mathalani, kijiji chenye wanafunzi takribani mia moja na sitini wanatumia tundu moja tu la choo na mabafu mawili. Hali hii inapelekea mlipuko wa magonjwa hatari kama vile U.T.I ( Urinary Tract Infection), kuhara na homa ya matumbo.
Licha ya malalamiko ya muda mrefu, uongozi washule umekuwa ukifumbia macho matatizo haya kwa kutoonesha jitihada za dhati kutokomeza mazingira haya hatarishi kwa afya zetu. Tumekuwa tukipokea ahadi zisizotekelezwa huku matatizo yakizidi kuongezeka ukubwa.
3.      Taaluma
Kwa hakika, taaluma ndio lengo kuu linalotuweka sisi wanafunzi shuleni. Tumekuwa tukivumilia tabia mbalimbali za walimu wetu ambazo zimekuwa kama mizaha juu ya hatima ya maisha yetu ya baadae. Tumekuwa tukifanya mitihani na baadae hucheleweshwa kurudishwa au wakati mwingine kutorudishwa kabisa. Na hata kama ikirudishwa, huwa hatufanyiwi masahihisho.
Pia, suala la uwajibikaji wa walimu limekuwa tatizo. Vipindi vya madarasani mara nyingi hupita bila kufundishwa. Ufundishaji wa walimu wengi umekuwa mbovu na wa kusuasua na hata wakati mwingine mitihani inayotungwa huwa haikidhi vigezo, na mingine hutolewa nje ya mfumo wa mtaala.
Tumekuwa tukivumilia tatizo la kukosa mahala tengwa kwa ajili ya mijadala ya kwenye vikundi (group discussions). Kila mara tulipojaribu kushauri, hata kushawishi tupewe mahali palipo tengwa kwa ajili ya mijadala hiyo tulijibiwa vibaya na hata kuzuiliwa kutumia baadhi ya sehemu za mazingira ya shule kwa shughuli yoyote ya kusoma, mfano: bwaroni.
Maktaba yetu ya shule haitunufaishi wanafunzi. Kumekuwa na utaratibu mbovu wa matumizi ya maktaba, na kwa muda mwingi maktaba yetu imekuwa ikibakia imefungwa tu. Uongozi wa shule umeshindwa kabisa kubuni namna nzuri ya kutumia maktba hiyo. Maktaba haifunguliwi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi nyakati za usiku badala yake hutumiwa tu na walimu pamoja na watu wengine wasio walimu wala wafanyakazi wa shule.
Licha ya hayo, maktaba yetu haina kabisa vitabu vya kisasa. Vitabu vilivyopo ni vya zamani ambavyo haviendani na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa. Aidha, uongozi wa shule haujawahi kuonesha juhudi zozote, hata kujadili nasi namna ya kutatua matatizo haya.
Pamoja na hayo, uongozi wa shule umekuwa ukipuuza mapendekezo ya kufanyika kwa shughuli za kitaaluma shuleni. Pamoja na kuzungushwa sana na kudhalilishwa sanakwa viongozi wetu wa serikali ya wanafunzi pindi wanapotaka majibu juu ya masuala hayo ya kitaaluma, milolongo mikubwa ya ufuatiliaji huibuliwa ili kusudi ikwamishe juhudi zetu, kwa mfano; Juma la uzungumzaji kiingereza (English Week) kama chachu ya kuhamasisha taaluma ya kuzungumza na kutumia kiingereza, uongozi ulicchangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maandalizi yake ikiwemo kukataa kutoa fedha za gharama za siku ya kilele chake.
Tumekuwa tukisifika Tanzania kote juu suala taaluma, lakini kwa miaka ya hivi karibuni taaluma ya shule imekuwa ikishuka kwa kasi. Kwa kiasi kikubwa, matatizo haya ambayo yamelelewa hadi kukomaa na uongozi wa shule uliopo yamechangia kushusha taaluma ya shule.
4.       Uwajibikaji
Uwajibikaji wa walimu hapa shuleni umekuwa tatizo kiasi cha kurudisha nyuma maendeleo ya shule. Ambapo, mkuu wa shule hatekelezi maoni yanayotolewa na wanafunzi. Pia amekuwa akitoa lugha chafu na kejeli pindi anaposhauriwa au kuombwa taarifa za kiutendaji. Mfano: “nyinyi wahuni”; “nyinyi watoto wa kike”. Katika hili amediriki pia wakati mwingine kuwadhalilisha hata walimu wenzake mbele ya wanafunzi.
Mkuu wa shule amekuwa akitoa majibu mepesi na wakati mwingine yasiyo na uhakika pale anapoulizwa habari ya masuala nyeti, mfano alipoulizwa juu ya taarifa ya mapato ya shule na kubainisha vyanzo vya mapato hayo, ambapo alidai kuwa hana muongozo unaomruhusu kufanya hivyo, ingawa baadae alikiri kuwa alifanya makosa kwa kutotoa taarifa hizo, huku akibabaika kubainisha vyanzo vyote vya mapato ya shule kwani alitaja baadhi tu vyanzo na kuficha vingine.
Mwalimu wa nidhamu naye ameshindwa kutimiza majukumu yake, hasa pale anapovuka mipaka na miiko ya maadili ya kazi yake kwa kuwashambulia wwanafunzi kwa ngumi na mateke na kutoa adhabu kubwa zilizopitiliza (Corporal Punishment).
Aidha, mwalimu huyo amekuwa na tabia ya kutoa lugha chafu za matusi (mifano tunayo) pamoja na kutoa vitisho mbalimbali.
Kwa ujumla, baadhi ya walimu wamekuwa na tabia ya kutofika shuleni kwa wakati na huondoka shuleni kabla ya mwisho wa saa za kazi, hususani walimu wa zamu na hili huchangiwa na kile kinachosemekana kuwa mwalimu wa somo husika hufundisha shule nyingine nje ya kituo chake cha kazi.
5.      Ukarabati na miundombinu ya shule
Majengo na miundombinu karibu yote hapa shuleni ni chakavu sana kiasi cha kuhatarisha maisha yetu hapa shuleni. Kumekuwa na uchakavu uliofumbiwa macho ikiwemo:-
o   Uchakavu wa mabweni na madarasa
o   Vyoo na mabafu yote
o   Jikoni, ambapo hali yake inatisha kiasi cha kuhatarisha usalama wa afya
o   Maabara
o   Taa za mabweni na madarasa
o   Viwanja vya michezo; mfano, mpira wa kikapu na mpira wa wavu
o   Kukosekana kwa mipira ya michezo
o   Ukosefu wa vifaa vya usafi kama vile mafagio, mafyekeo, dawa za kusafishia vyoo, na madekio hali inayopelekea wanafunzi kuwa na hali ngumu wakati wa kufanya usafi
6.      Chakula
Chakula ni mahitaji makuu na ya msingi kwa mwanadamu yeyote. Ni dhahiri kwamba chakula tunachopatiwa hakikidhi viwango kiafya na hilo limedhibitishwa kuwa kutokana na ubadhirifu katika fungu linalotengwa kwa ajili ya chakula. Mfano mzuri ni kutopewa mbogamboga, kulishwa ugali mchungu na unaonuka na wakati mwingine usioiva. Wali unaotokana na mchele ulionyeshewa/uliolowa na hata kulishwa maharage yasiiokidhi kiwango na zaidi ya yote ubadhirifu huu hupelekea chakula kuwa kidogo na kisichotosha


7.      Ulinzi na usalama
Tumekuwa tukikabiliwa na matatizo ya kuibiwa mali zetu hii hutokana na kuwa na walinzi tulionao kuwa wachache hivyo hawawezi kulinda eneo lote la shule. Katika bweni moja (Karume 6) wanafunzi wanafunzi waliibiwa mabegi yao na watu wasiowanafunzi. Tumekuwa tukiibiwa mali zetu mara kwa mara bila uongozi wa shule kutoa maelezo au kuonesha jitihada zozote za kukomesha hali hii.
HITIMISHO:
Mwisho, sisi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe kutokana na hali mbaya ya miundombinu kama vile vyoo, mabafu, mabweni na madarasa na hali mbaya ya chakula hatupo tayari kuendelea kuishi katika mazingira haya hatarishi. Mazingira mabovu ya kujisomea pamoja na uongozi mbaya na mbovu haviwezeshi maisha yetu kuwa ya amani shuleni. Hivyo basi, hatuutaki uongozi mzima wa shule ya Sekondari Mzumbe uliopo sasa. Tunamtaka mkuu wa shule pamoja na safu yake yote waondolewa na tupatiwe mkuu wa shule mwingine. Kwasasa hatupo tayari kuendelea kuwepo shuleni mpaka pale miundombinu itakapo karabatiwa na kufaa tena kuishi binadamu.



“TOMORROW’S FUTURE DEPENDS ON WHAT WE IMPLANT TODAY”




“DETERMINATION IS OUR MOTTO”
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Mzumbe
29.05.2013
















UCHAKAVU WA MUINDOMBINU KAMA HII NI MOJA YA SABABU ZILIZOLETEA MGOMO HUU

  


Uchakavu wa mabweni kama inavyoonekana hapa ni moja ya sababu zilizoletea maandamano hayo ya wanafunzi wa mzumbe sekondari.
https://www.jamiiforums.com/attachment.php?attachmentid=95557

MABWENI YA SHULE HII NI YALEYALE YALIYOKUWA YAKITUMIKA TANGU ENZI ZA WAKOLONI.. JE SERIKALI IMEISAHAU SHULE HII MAALUM KABISAA??