Idadi ya
watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati
ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya
marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi
limebaini.
Habari ambazo gazeti hili
imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na
kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale
ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka
Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la
kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa
awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao
82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa
wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo
mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa
wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa
225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo
walifaulu.
Msemaji wa Necta, John
Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua
kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili
watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema
Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa
mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya
awali
Matokeo ya awali
yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne
mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa
126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa
na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo,
watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo
imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja
hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka
Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya
kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500
kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.