UTANGULIZI
Shule ya
sekondari Mzumbe ni moja kati ya shule
maalumu nchini Tanzania. Ni shule ambayo inasfika kote Tanzania kwa taaluma na
nidhamu yake safi. Kwa kuthibitisha hayo, viongozi wengi bora wa serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni matunda ya shule hii.
Kwa sifa
hiyo,sisi wanafunzi wa shule ya sekondari Mzumbe tunajivunia kuwepo shuleni
hapa na tunajitahidi kutimiza wajibu wetu ili kutunza na kuendeleza sifa ya
shule hii kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla. Tukiwa na wajibu huo mzito,
tunahitaji mazingira bora ya kujifunzia kama vile vifaa na nyenzo bora za
kitaaluma, uongozi bora na ushirikiano chanya baina ya wanafunzi na walimu.
Hata hivyo,
hali ya maisha ya hapa shuleni kwa sasa inazidi kuwa mbaya kiasi cha kuwa
kipingamizi katika juhudi za kutimiza malengo yetu, katika kutimiza malengo
yetu ya kulijenga taifa kama yalivyo matumaini ya watanzania wote.
Pamoja na
hali hiyo tumejitahidi kukabiliana na matatizo mengi yaliyopo kwa njia
mbalimbali hususani kufanya mazungumzo na kushauriana na uongozi wa shule kwa
kuzingatia itifaki bila ya mafanikio yoyote.
Kutokana
hali hiyo, sisi wanafunzi wa shule ya sekondari Mzumbe tumefikia uamuzi wa
kuandika waraka unaoeleza matatizo yanayotukabili ambayo tumeyabainisha katika
vipengele vifuatavyo:
1.
Mapato na matumizi ya shule
Kama
wanafunzi tuna haki ya kushirikishwa katika taarifa za mapato na matumizi ya
shule yetu. Shule ina vyanzo mbalimbali vya mapato kama vile ukumbi wa shule
unaokodishwa kwa ajili ya sherehe mbalimbali, ushuru kutoka katika magenge na
maduka (soko la Mzumbe sekondari), mashamba yanayokodishwa, ada ya kituo kwa
wanafunzi wanaorudia mitihani pamoja na
kituo cha masomo ya jioni kilichopo ndani ya eneo la shule (Mzumbe evening
class). Pamoja na hayo, hatupewi taarifa
juu ya pesa zinazotokana na miradi hiyo.
Kutokana na
hali hiyo, tumebaini kuwa kutotolewa kwa taarifa ya mapato na matumizi
kumesababisha ubadhilifu na ufisadi
unaoendelea hapa shuleni.
2.
Afya
Ni wazi
kuwa, afya bora ni muhimu kawa mwanadamu yoyote ili aweze kutimiza wajibu wake.
Lakini kwa sasa suala la afya limekuwa tatizo kubwa hapa shuleni. Mfano: utaratibu
mbovu wa matibabbu, ambapo kuna mlolongo mrefu sana katika ufuatiliaji wa
huduma za matibabu, ikiwemo kutotolewa kwa fedha za matibabu haliinayotulazimu
kutumia fedha zetu za mifukoni ambazo hatahivyo huwa
hatulipwi, licha ya kuwa tulikwisha lipia awali f edha za matibabu.
Kukosekana
kwa dawa hata zile za muhimu katika zahanati ya shule limekuwa tatizo
sugu.Hivyo, tumekuwa tukilazimika kununua dawa katika maduka ya madawa.
Kutokana na
ubovu na uchakavu wa zahanati yetu, hali ya zahanati hiyo ni ya kusikitisha
sana, kwani inashindikana hata kutoa
huduma ndogo ndogo za kiafya.
Pia, hali
mbaya ya vyoo na mabafu yetu ni tishio kwa afya zetu. Mathalani, kijiji chenye
wanafunzi takribani mia moja na sitini wanatumia tundu moja tu la choo na
mabafu mawili. Hali hii inapelekea mlipuko wa magonjwa hatari kama vile U.T.I (
Urinary Tract Infection), kuhara na homa ya matumbo.
Licha ya
malalamiko ya muda mrefu, uongozi washule umekuwa ukifumbia macho matatizo haya
kwa kutoonesha jitihada za dhati kutokomeza mazingira haya hatarishi kwa afya
zetu. Tumekuwa tukipokea ahadi zisizotekelezwa huku matatizo yakizidi
kuongezeka ukubwa.
3.
Taaluma
Kwa hakika,
taaluma ndio lengo kuu linalotuweka sisi wanafunzi shuleni. Tumekuwa
tukivumilia tabia mbalimbali za walimu wetu ambazo zimekuwa kama mizaha juu ya
hatima ya maisha yetu ya baadae. Tumekuwa tukifanya mitihani na baadae hucheleweshwa
kurudishwa au wakati mwingine kutorudishwa kabisa. Na hata kama ikirudishwa,
huwa hatufanyiwi masahihisho.
Pia, suala
la uwajibikaji wa walimu limekuwa tatizo. Vipindi vya madarasani mara nyingi
hupita bila kufundishwa. Ufundishaji wa walimu wengi umekuwa mbovu na wa
kusuasua na hata wakati mwingine mitihani inayotungwa huwa haikidhi vigezo, na
mingine hutolewa nje ya mfumo wa mtaala.
Tumekuwa
tukivumilia tatizo la kukosa mahala tengwa kwa ajili ya mijadala ya kwenye
vikundi (group discussions). Kila mara tulipojaribu kushauri, hata kushawishi
tupewe mahali palipo tengwa kwa ajili ya mijadala hiyo tulijibiwa vibaya na
hata kuzuiliwa kutumia baadhi ya sehemu za mazingira ya shule kwa shughuli
yoyote ya kusoma, mfano: bwaroni.
Maktaba yetu
ya shule haitunufaishi wanafunzi. Kumekuwa na utaratibu mbovu wa matumizi ya
maktaba, na kwa muda mwingi maktaba yetu imekuwa ikibakia imefungwa tu. Uongozi
wa shule umeshindwa kabisa kubuni namna nzuri ya kutumia maktba hiyo. Maktaba
haifunguliwi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi nyakati za usiku badala yake
hutumiwa tu na walimu pamoja na watu wengine wasio walimu wala wafanyakazi wa
shule.
Licha ya
hayo, maktaba yetu haina kabisa vitabu vya kisasa. Vitabu vilivyopo ni vya
zamani ambavyo haviendani na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa.
Aidha, uongozi wa shule haujawahi kuonesha juhudi zozote, hata kujadili nasi
namna ya kutatua matatizo haya.
Pamoja na
hayo, uongozi wa shule umekuwa ukipuuza mapendekezo ya kufanyika kwa shughuli
za kitaaluma shuleni. Pamoja na kuzungushwa sana na kudhalilishwa sanakwa
viongozi wetu wa serikali ya wanafunzi pindi wanapotaka majibu juu ya masuala
hayo ya kitaaluma, milolongo mikubwa ya ufuatiliaji huibuliwa ili kusudi
ikwamishe juhudi zetu, kwa mfano; Juma la uzungumzaji kiingereza (English Week)
kama chachu ya kuhamasisha taaluma ya kuzungumza na kutumia kiingereza, uongozi
ulicchangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maandalizi yake ikiwemo kukataa kutoa
fedha za gharama za siku ya kilele chake.
Tumekuwa
tukisifika Tanzania kote juu suala taaluma, lakini kwa miaka ya hivi karibuni
taaluma ya shule imekuwa ikishuka kwa kasi. Kwa kiasi kikubwa, matatizo haya
ambayo yamelelewa hadi kukomaa na uongozi wa shule uliopo yamechangia kushusha
taaluma ya shule.
4.
Uwajibikaji
Uwajibikaji
wa walimu hapa shuleni umekuwa tatizo kiasi cha kurudisha nyuma maendeleo ya
shule. Ambapo, mkuu wa shule hatekelezi maoni yanayotolewa na wanafunzi. Pia
amekuwa akitoa lugha chafu na kejeli pindi anaposhauriwa au kuombwa taarifa za
kiutendaji. Mfano: “nyinyi wahuni”; “nyinyi watoto wa kike”. Katika hili
amediriki pia wakati mwingine kuwadhalilisha hata walimu wenzake mbele ya
wanafunzi.
Mkuu wa
shule amekuwa akitoa majibu mepesi na wakati mwingine yasiyo na uhakika pale
anapoulizwa habari ya masuala nyeti, mfano alipoulizwa juu ya taarifa ya mapato
ya shule na kubainisha vyanzo vya mapato hayo, ambapo alidai kuwa hana muongozo
unaomruhusu kufanya hivyo, ingawa baadae alikiri kuwa alifanya makosa kwa
kutotoa taarifa hizo, huku akibabaika kubainisha vyanzo vyote vya mapato ya
shule kwani alitaja baadhi tu vyanzo na kuficha vingine.
Mwalimu wa
nidhamu naye ameshindwa kutimiza majukumu yake, hasa pale anapovuka mipaka na
miiko ya maadili ya kazi yake kwa kuwashambulia wwanafunzi kwa ngumi na mateke
na kutoa adhabu kubwa zilizopitiliza (Corporal Punishment).
Aidha,
mwalimu huyo amekuwa na tabia ya kutoa lugha chafu za matusi (mifano tunayo)
pamoja na kutoa vitisho mbalimbali.
Kwa ujumla,
baadhi ya walimu wamekuwa na tabia ya kutofika shuleni kwa wakati na huondoka
shuleni kabla ya mwisho wa saa za kazi, hususani walimu wa zamu na hili
huchangiwa na kile kinachosemekana kuwa mwalimu wa somo husika hufundisha shule
nyingine nje ya kituo chake cha kazi.
5.
Ukarabati na miundombinu ya shule
Majengo na
miundombinu karibu yote hapa shuleni ni chakavu sana kiasi cha kuhatarisha
maisha yetu hapa shuleni. Kumekuwa na uchakavu uliofumbiwa macho ikiwemo:-
o
Uchakavu
wa mabweni na madarasa
o
Vyoo
na mabafu yote
o
Jikoni,
ambapo hali yake inatisha kiasi cha kuhatarisha usalama wa afya
o
Maabara
o
Taa
za mabweni na madarasa
o
Viwanja
vya michezo; mfano, mpira wa kikapu na mpira wa wavu
o
Kukosekana
kwa mipira ya michezo
o
Ukosefu
wa vifaa vya usafi kama vile mafagio, mafyekeo, dawa za kusafishia vyoo, na
madekio hali inayopelekea wanafunzi kuwa na hali ngumu wakati wa kufanya usafi
6.
Chakula
Chakula ni
mahitaji makuu na ya msingi kwa mwanadamu yeyote. Ni dhahiri kwamba chakula
tunachopatiwa hakikidhi viwango kiafya na hilo limedhibitishwa kuwa kutokana na
ubadhirifu katika fungu linalotengwa kwa ajili ya chakula. Mfano mzuri ni
kutopewa mbogamboga, kulishwa ugali mchungu na unaonuka na wakati mwingine
usioiva. Wali unaotokana na mchele ulionyeshewa/uliolowa na hata kulishwa
maharage yasiiokidhi kiwango na zaidi ya yote ubadhirifu huu hupelekea chakula
kuwa kidogo na kisichotosha
7.
Ulinzi na usalama
Tumekuwa
tukikabiliwa na matatizo ya kuibiwa mali zetu hii hutokana na kuwa na walinzi
tulionao kuwa wachache hivyo hawawezi kulinda eneo lote la shule. Katika bweni
moja (Karume 6) wanafunzi wanafunzi waliibiwa mabegi yao na watu
wasiowanafunzi. Tumekuwa tukiibiwa mali zetu mara kwa mara bila uongozi wa
shule kutoa maelezo au kuonesha jitihada zozote za kukomesha hali hii.
HITIMISHO:
Mwisho, sisi
wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe kutokana na hali mbaya ya miundombinu
kama vile vyoo, mabafu, mabweni na madarasa na hali mbaya ya chakula hatupo
tayari kuendelea kuishi katika mazingira haya hatarishi. Mazingira mabovu ya
kujisomea pamoja na uongozi mbaya na mbovu haviwezeshi maisha yetu kuwa ya
amani shuleni. Hivyo basi, hatuutaki uongozi mzima wa shule ya Sekondari Mzumbe
uliopo sasa. Tunamtaka mkuu wa shule pamoja na safu yake yote waondolewa na
tupatiwe mkuu wa shule mwingine. Kwasasa hatupo tayari kuendelea kuwepo shuleni
mpaka pale miundombinu itakapo karabatiwa na kufaa tena kuishi binadamu.
“TOMORROW’S FUTURE DEPENDS ON WHAT WE IMPLANT TODAY”
“DETERMINATION IS OUR
MOTTO”
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Mzumbe
29.05.2013
No comments:
Post a Comment