Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametolea ufafanuzi kuhusu mswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba mpya na kusema umakini na uaminifu unahitajika katika kujadili mswada huo ili pale mapungufu yatakapobainika yaondolewe kwa manufaa ya taifa.
Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni Dodoma, Waziri Mkuu Pinda amesema hatua ya wabunge kutoka nje ya bunge kwa madai ya kutoafiki baadhi ya vipengele vya mswada sio sahihi kwani swala lililopo ni kuujadili mswada husika na kurekebisha dosari zitakazobainika.
Kipindi cha maswali na majibu bungeni, hoja kubwa zimeulizwa na wabunge na kutolewa majibu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Kiongozi wa kambi ya rasmi ya upinzani Freeman Mbowe ameshauri kwamba kabla ya mjadala wa mswada wa mabadiliko ya katiba mpya kuwasilishwa bungeni ungepitiwa kwanza ili kutoa dosari, hoja ambayo imeungwa mkono na Waziri Mkuu.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum James Mbatia ameeelezea mapungufu yaliyomo katika Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Waziri Mkuu Pinda amesema mapungufu yote hayo yataondolewa baada ya kupitishwa kwa katiba mpya.
Suala la uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam nalo lilmeibuka ambapo Waziri Mkuu akatoa maelezo ikiwemo upanuzi wa bandari hiyo, reli kwa ajili ya kuchukua mizigo bandarini kwenda mikoani na nje ya nchi pamoja na kukiboresha kitengo cha makontena ili kupunguza mrundikano wa mizigo.
Ulipofika wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana ya mazingira Dokta Thereza Huviza akaelezea kilio cha wananchi wa eneo la Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam kuhusu madhara yanayotokana na hewa inayotoka kwenye matenki ya kuhifadhia mafuta.
Aidha Dokta Huviza ameyataja mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa ya Ukaa - MKUHUMU kuwa ni pamoja na kulipwa fedha za kutunza misitu na ufadhili unaotolewa kwa wanafunzi wanaochukua kozi za uzamili na uzamivu katika hifadhi ya mazingira.
Mkutano wa Kumi na Mbili Kikao cha nane unaendelea mjini Dodoma ambapo leo wabunge wanajadili mswada wa mabadiliko ya katiba mpya.
Dominick Mokiwa, TBC Dodoma.
No comments:
Post a Comment